Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, tawala za Aal Saud na Aal Khalifa, wakitumia kivuli cha vita vya Ghaza, mazungumzo kuhusu makubaliano ya kusitisha vita na misaada kwa watu wa Ghaza pamoja na juhudi za kuvunja mzingiro, wameongeza shinikizo, dhulma, na hukumu za kunyonga dhidi ya jamii za Kishia nchini Saudi Arabia na Bahrain.
Katika wiki za hivi karibuni, taarifa zimeenea kuhusu kukamatwa na kunyongwa kwa wafungwa waliokuwa katika magereza ya utawala wa Saudia.
Shahidi Muhammad Hasan Al-Ammar (Abu Fatoum) — mpiganaji na mwenye subira — baada ya safari iliyojaa uvumilivu, uthabiti, na imani, safari ambayo aliitumia katika kutetea wanyonge, kushikamana na haki, kumwamini Mola wake, na kutumaini radhi Zake, roho yake safi ilipaa kuelekea kwa Muumba wake katika mji wa Awamiyah, ulioko katika Mkoa wa Mashariki ya Saudi Arabia. Utawala huu wa kifahari na dhalimu wa Saudia umetenda tena jinai ya kutisha – jinai inayotikisa dhamiri za watu huru na kuzitia huzuni nyoyo za waumini.
Shahidi huyo mwenye heri alikuwa mfano bora wa uchamungu na unyenyekevu, kielelezo safi cha imani na uimara mbele ya majaribu. Katika kila mtihani alikuwa akitafuta thawabu. Hata akiwa gerezani, kama mtu huru, alikuwa akimkumbuka Mola wake; hakuwahi kuacha faradhi wala sunna yoyote. Mwili wake ulikuwa gerezani, lakini roho na imani yake zilikuwa huru. Amewaacha mabinti watatu wadogo, mkubwa wao akiwa na umri wa miaka kumi na tatu pekee.
Jumuiya ya “Amal al-Islamiyyah” ya Bahrain, katika tamko lake, imelaani vikali jinai ya utawala wa Saudia ya kumuua shahidi Muhammad Husayn Al-Ammar kutoka mji wa Qatif, na kuutaja utawala huo kuwa ndio unaobeba dhamana kamili ya jinai hii ya kutisha.
Tamko hilo linasema:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
“Wala kabisa usiwadhanie walio uliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti. Bali hao ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi..”
Amesema kweli Mwenyezi Mungu Aliye juu na Mtukufu.
Utawala wa Saudia, katika sura mpya ya ukandamizaji wa kimfumo, ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu, na kutojali uhai wa raia wa Kishia, mnamo asubuhi ya Alhamisi tarehe 9 Oktoba 2025, umetekeleza hukumu ya kumnyonga Muhammad Husayn Al-Ammar, kijana wa mji wa Awamiyah katika Mkoa wa Qatif — baada ya miaka mingi ya kifungo na mateso katika magereza ya Saudia, kupitia mahakama zisizo na hata viwango vya chini vya haki na uaminifu.
Tamko hilo linaendelea kisema: Sisi, Jumuiya ya Amal al-Islamiyyah ya Bahrain, tunalaani kwa maneno makali kabisa jinai hii ya kutisha, inayodhihirisha ukweli wa udikteta na dhulma zinazofanywa na utawala wa Saudia dhidi ya dhehebu la Kishia, na kufichua uongo wa kauli zake kuhusu “mageuzi” na “haki”.
Hukumu hizi za vifo vya kisiasa, zinazotekelezwa nje ya muktadha wa kesi za haki, si chochote ila ni nyenzo za kusambaza hofu na kuzinyamazisha sauti za watu huru. Hazina uhalali wowote chini ya hali yoyote ile — hasa zikizingatia kuwa zimeelekezwa dhidi ya vijana waliokuwa wakipigania haki zao halali za hadhi, uadilifu, na uhuru.
Tunautaja utawala wa Saudia kuwa unawajibika kikamilifu katika jinai hii na kwa kila tone la damu lililomwagwa kwa dhulma na ujeuri. Tunasisitiza kuwa jinai hizi haziwezi kuzinyamazisha sauti za watu huru, bali zitazidisha azma na dhamira yao ya kuendelea katika njia ya uhuru, kutetea heshima ya binadamu, na kujikomboa kutokana na alama za dhulma na ukosefu wa haki.
Mwisho, tunatoa salamu za rambirambi na faraja za dhati kwa familia ya shahidi Muhammad Husayn Al-Ammar, pamoja na watu mashujaa wa Awamiyah na Qatif. Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amrehemu shahidi huyo kwa rehema Zake pana, na awape watu wetu uhuru, haki, usawa, na ushindi wa karibu.
Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na hakika sisi kwake yeye ni wenye kurejea
Maoni yako